Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wazalendo Huru Dkt. Mohamed Mwampogwa ameiomba Serikali kupunguza bei ya Gesi, ili familia zote ziweze kushiriki kampeni za kutunza mazingira kwa kutumia Nishati hiyo badala ya kuni na mkaa.
Mwampogwa ameyasema hayo katika zoezi la upandaji miti lilolofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mwakamo na Sekondari ya Samia Mtongani, katika Kijiji cha Kisabi kilichopo Mlandizi Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema, matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ni makubwa nchini, hivyo ili kunusuru hali hiyo Watanzania wanapaswa kupika kwa kutumia nishati safi ya Gesi badala ya kuni na mkaa ambayo itasababisha uendelevu wa ukataji miti na kuharibu mazingira.
“Matumizi ya kuni na mkaa nchini ni makubwa sana na kupelekea kuendelea kuharibu mazingira yetu kwani kuni na mkaa hutokana na miti ya misitu yetu hivyo tutaokoa mazingira yetu,” alisema Mwampogwa.
Kuhusu zoezi la upandaji miti, amesema jumla ya Miche 300 imepandwa katika Shule mpya ya Msingi Mwakamo na Sekondari ya Samia Mtongani ikiwa ni jitihada za kuunga mkono utunzaji wa mazingira.
Mwampogwa amesema miti iliyopandwa ni ya Matunda, Vivuli na Mbao huku akisema zoezi hilo ni endelevu kwani tayari wamelitekeleza katika maeneo mbalimbali Nchini kauli ambayo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Yahya Calamba.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo la Wazalendo huru Taifa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa hilo mkoa wa Pwani, Hadija Juma amesema Taifa lipo katika wiki ya mazingira na wao wamechagua shule hizo mbili ili ziwe za mfano.
Amesema upandaji miti huo pia ni sehemu ya sherehe za kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa hilo kwani mwezi huu (Machi 2024), anatarajia kutunukiwa Nishani ya Udaktari wa heshima, kwa kazi nzuri anazoendelea kuzifanya nchini.