Idadi ya watu waliokufa kwenye shambulizi la la silaha lililodaiwa kufanywa na wapiganaji wa Islamic State, lililotokea usiku wa kuamkia leo Machi 23, 2024 nchini Urusi, imefikia watu 115 wakiwemo watoto watatu, huku wengine zaidi ya 139 wakijeruhiwa.

Inadaiwa kuwa washambuliaji waliingia kwenye Ukumbi wa Crocus uliopo Krasnogorsk kaskazini-magharibi mwa jiji la Moscow, wakiwa wameficha nyuso zao na kuanza kufyatua hovyo risasi pamoja na kurusha mabomu yaliosababisha kuzuka kwa moto.

Tayari watu 11 ikiwemo wanne wanaoshukiwa kufanya shambulizi hilo wamekamatwa, huku kundi linalojiita dola la Kiislamu – IS, likidai kuhusika na shambulio hilo baya zaidi kutokea nchini Urusi.

Waziri wa afya Urusi, Mikhail Murashko amesema watu kadhaa wamelazwa Hospitalini wakiwemo watoto huku mmoja kati ya hao akiwa katika hali mahututi na uchunguzi wa wa tukio hilo umeanza huki rais Vladimir Putin akipokea taarifa za kila wakati.

Kufuatia tukio hilo, Viongozi wa dunia toka Mataifa mbalimbali wamelaani kwa matamshi makali shambulizi hilo huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kupitia msemaji wake Farhan Haq akituma salamu za pole kwa familia za waathirika na Serikali ya Urusi.

Wengine waliotuma Salaam za Ole ni Ikulu ya Marekani, Rais Xi Jinping wa China ambaye ni mshirika wa karibu wa Urusi, Viongozi wa Ujerumani, Japan, Italia, Belarus, Mexico na Venezuela na Umoja wa Ulaya wakisema wameshtushwa na shambulio hilo.

Ikumbukwe kuwa, Machi 7, 2024 ubalozi wa Marekani jijini Moscow ulitoa tahadhari ya usalama, baada ya kupokea ripoti kwamba watu wenye itikadi kali wana mipango ya kushambulia mikusanyiko mikubwa mjini Moscow, ikiwemo matamasha.

 

Watumishi Bandari kuchagua kati ya TPA au DP World
Ulinzi wa Mazingira: Serikali yaombwa kupunguza bei ya Gesi