Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema kila aliyehusika kwenye shambulizi lililowaua Watu zaidi ya 100 hadi sasa katika eneo la Crocus City Hall Nchini Urusi, atakumbana na adhabu kali ambapo amesisitiza kuwa watamshughulikia kuanzia aliyewatuma hadi waliotekeleza uhalifu huo.
Akihutubia Wananchi wa Urusi hii leo, Putin ameliita shambulizi hilo kuwa ni la damu na la kishenzi ambapo amesema kwa sasa nguvu kubwa inaelekezwa kwenye kuwazuia walio nyuma ya shambulizi hilo wasifanye uhalifu mwingine huku pia akitoa pole kwa wote walioguswa na kuumizwa na vifo na majeruhi yaliyotokana na shambulizi hilo.
Shambulizi hilo la kigaidi, ambalo Kikundi cha Kigaidi cha ISIS kimedai kuhusika nalo, limetokea usiku wa kuamkia leo ambapo Vijana walioficha sura zao waliwashambulia Watu kwa risasi na kulipua jengo hilo.
Mapema hapo jana (Machi 23, 2024), Mamlaka za usalama Nchini Urusi zilimfahamisha Rais Putin kwamba zimewakamata Watu 11 wakiwemo wanne ambao wamehusika moja kwa moja na shambulizi hilo, Watu hao wamekamatwa wakiwa wanavuka mpaka wa Urusi na Ukraine na walikuwa na mawasiliano na upande wa Ukraine.