Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo Jumatatu (Machi 25), kitashuka tena kwenye Uwanja wa Dalga Arena nchini Azerbajjan kucheza dhidi ya Mongolia katika mechi ya mashindano maalum ya FIFA Series 2024 yanayoendelea nchini humo.
Stars itakuwa inajaribu bahati yake baada ya mechi ya kwanza ljumaa (Machi 22) kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria katika mfululizo wa michezo ya michuano hiyo.
Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amewahakikishia watanzania kuwa katika mechi ya leo Jumatatu (Machi 25) wanatarajia kuibuka na ushindi kwani haiwezekani wapoteze michezo miwili mfululizo.
“Tumebakiwa na mchezo mmoja ambao ni huu, mechi iliyopita tulipoteza ila kiwango kilikuwa kizuri, kwangu mimi si kitu chenye tija kuona tunapoteza mechi zote mbili.
“Tumekaa na wachezaji tukaangalia mapungufu ya mechi ya kwanza, tumeyarekebisha, Mongolia nimeiangalia kiwango chake ni kama Bulgaria tu, tunawaheshimu, lakini tunahitaji kupata matokeo ya ushindi, tunahitaji kuongeza nguvu. tunajipanga kwenda kupambana,” amesema Morocco.
Feisal Salum amewaahidi watazania ushindi katika mechi ya leo Jumatatu (Machi 25) kwani wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi iliyopita.
“Sisi kama wachezaji tuko vizuri, nilikosa mabao kwenye mchezo uliopita haikuwa bahati yangu, ila nawaahidi katika mchezo huu nikipata nafasi nzuri nitafunga, na nawaahidi watanzania ushindi.
Katika mechi ya ljumaa (Machi 22), Fei Toto alikuwa miongoni mwa wachezaji walioikosesha Stars mabao matatu ya wazi, ambapo alipiga juu akiwa na kipa, huku pia akiwa na uwezo wa kumpasia Kibu Denis aliyekuwa kwenye eneo zuri zaidi.
Kibu naye alikosa bao la wazi dakika ya 20, kwa kugongesha nguzo ya pembeni, akiwa amebaki na kipa Dimitar Mitov wa Bulgaria, na Clement Mzize akigongesha mwamba wa juu katika dakika ya 90 ya mchezo kwennye mechi hiyo ambayo Stars ililala kwa bao 1-0.