Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Nchini, Nassor Hamdoun, ameunga mkono tamko la Shirikisho la Soka Nchini ‘TFF’ kuwa msimu ujao Ligi Kuu Tanzania Bara itatumia teknolojia ya kuwasaidia waamuzi ‘VAR’ kwa baadhi ya mechi, huku pia akipongeza kuwepo kwa waamuzi kutoka nje ya nchi watakaochezesha baadhi ya mechi.
Hamdoun amesema baada ya Rais wa TFF, Wallace Karia kutamka rasmi kuwa msimu ujao kwa mara ya kwanza, Ligi Kuu itatumia VAR mbili kwa ajili ya kusaidia waamuzi, moja ikiwa ni msaada kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika ‘CAF’, na nyingine itanunuliwa na mmoja wa wadhamini wa Ligi Kuu waliopewa haki ya kuonyesha michezo ya ligi kwenye televisheni ambao wataleta VAR inayohamishika ‘Mobile VAR.’
Hamdoun pia aliunga mkono wazo la kuwatumia waamuzi kutoka nje ya nchi akisema italeta chachu na kuwafanya hata waamuzi wa hapa nchini kuwa makini na uchezeshaji wao.
“Rais Karia ametamka wazi kuwa tukijaaliwa msimu ujao tutakuwa na VAR na sisi tunamuunga mkono kwa hilo jambo na tunampongeza kwa niaba ya Kamati ya Waamuzi, tunaomba alisimamie hilo ili kuondoa sintofahamu iliyokuwa inajitokeza viwanjani, sasa marefa wana uwezo wa kurudia kuangalia tukio na kujiridhisha kabla ya kutoa maamuuzi sahihi.
“Tutambue kuwa VAR ni moja kati ya nyenzo zitakazotusaidia sana kwenye uamuzi na waamuzi wetu kufanya maamuzi sahihi pale ambapo hawakuliona vizuri tukio ambapo kwa sasa hawawezi kufanya hivyo,” amesema Hamdoun
Hivi karibuni, TFF, pamoja na kukubali kuipokea timu ya Al Hilal ya Sudan, ilikiri pia kupokea waamuzi, ambao mpango ni kutaka wachezeshe soka nchini kwenye michezo mbalimbali, ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
“Tukumbuke mahusiano kutoka nje ni moja ya jambo bora katika kuwaendeleza waamuzi wetu, kumekuwa na taarifa ambazo zimeshatolewa ufafanuzi na TFF kwamba kuna waamuzi kutoka nje ya nchi wapo hapa na wenyewe watajumuishwa kwenye ligi yetu, nawahakikishia wadau na wao wenyewe kuwa tutakuwa nao, niwaombe waamuzi wenzangu wasione kama vile wanaingiliwa, hapana.”
“Hii ni changamoto ni lazima wakubaline nayo, tushirikiane nao kwa namna ya kuwaongezea wao kitu na sisi pia kupata kitu kutoka kwao, wote tujifunze, tunaunga mkono hilo,” amesema Bosi huyo wa Waamuzi.