Huku kukiwa na majadiliano juu ya kuhamia Real Madrid, Mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe amesema kwamba bado ana matumaini ya kushiriki michezo ya Olimpiki ya Paris msimu huu wa joto na kwamba hakuna mtu ambaye bado amemwambia hataweza kushiriki.
Mbappe anatarajiwa kujiunga na Madrid wakati mkataba wake na PSG utakapomalizika msimu huu wa joto, huku ESPN ikiripoti mwezi uliopita kuwa miamba hao wa La Liga wana matumaini ya kukamilisha makubaliano na mchezaji huyo hivi karibuni.
ESPN imegundua kuwa Real Madrid ilituma barua pepe kwa Shirikisho la Soka la Ufaransa mapema mwezi huu ikieleza kwamba haitamwachia mchezaji wao yeyote ili ashiriki kwenye michezo ya Olimpiki.
“Siku zote nilikuwa na nia sawa. Nimekuwa nikisema kwamba nilitaka kwenda kwenye Olimpiki, lakini hainitegemei mimi,” alisema Mbappe katika mkutano na waandishi wa habari.
“Siwezi kusema chochote kwa sababu hakuna aliyeniambia chochote. Ikiwa siwezi kushiriki Olimpiki iwe hivyo.
“Ninaposema hakuna mtu aliyeniambia chochote, nazungumzia PSG. Nina mkataba na PSG na hawajasema lolote kuhusu Olimpiki. Hatujaijadili,” aliongeza.
Nahodha huyo wa Ufaransa alikataa kuzungumzia mustakabali wake kwa klabu hiyo, lakini akasema anatarajia suluhu kabla ya majira ya joto.
“Bado sijatangaza chochote kwa sababu sina cha kutangaza nasikitika sina cha kukuambia,” alisema, kabla ya kuongeza baadaye: “Nadhani yote yatatatuliwa kabla ya Euro 2024.”
Mchezaji huyo wa PSG hakuwahi kuitaja Real Madrid wakati wa mkutano na waandishi wa habari, lakini mazungumzo kati ya kambi ya Mbappe na viongozi hao wa La Liga yanaendelea, chanzo kiliiambia ESPN.