Kiungo kutoka nchini Uganda Khalid Aucho amerejea uwanjani na leo Jumatatu (Machi 25) alitarajiwa kuanza mazoezi na kikosi kizima cha Young Africans baada ya kufuzu vipimo vya uponaji wa jeraha la upasuaji mdogo wa goti aliofanyiwa hivi karibuni na kumkosesha mechi nne za Ligi.

Aucho aliyeumia katika mechi ya mwisho ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, alikosa mechi za ligi dhidi ya Namungo, Ihefu na Geita Gold ambapo Young Africans ilishinda kwa kishindo na ile ya Azam FC iliponyooshwa mabao 2-1 Kwa Mkapa.

Kiungo huyo raia wa Uganda, alikuwa na mazoezi makali ya siku tisa na Youssef ambaye ni daktari wa viungo ambapo wikiendi iliyopita alimaliza taratibu zote za vipimo na sasa anajumuishwa na wenzake ukisalia uamuzi wa kocha Miguel Gamondi kumtumia kwenye mechi ijayo.

Mbali na Aucho pia beki Ibrahim Hamad ‘Bacca’, viungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Clement Mzize ambao walirejea nchini kutoka kambi ya timu ya Taifa Stars nao wataanza maandalizi hayo na wenzao.

Young Africans itakutana na Mamelodi katika mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Jumamosi (Machi 30) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya timu hizo kurudiana Aprili 5 mjini Pretoria, Afrika Kusini na mshindi wa jumla atasonga mbele kwa kutinga Nusu Fainali ya michuano hiyo.

Ally Salim: In Shaa Allah Al Ahly anang’oka
Mbappe: Ndoto zangu hazitayeyuka