Serikali Nchini, imesema itaendelea kuhakikisha inawezesha mazingira bora na rafiki kwa Vijana wabunifu kwa kutoa mikopo, ajira na kuwapa fursa mbalimbali kwa kutumia taaluma vyema katika kung’amua fursa katika jamii.
Hayo yamezungumzwa katika Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali, na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli, kwa hadhira iliyohudhuria tukio hilo Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro.
Amesema kuna dhana kuwa wasomi wengi wanahisi Serikali haiwasaidii kupata ajira lakini si kweli na kuwataka wasomi kutumia taaluma zao kubuni bunifu mbalimbali, kuendana na soko la ajira na kubadilisha mtazamo uliopo wa kusubiri ajira za Serikali kwani nguvu, fikra na mtazamo wa kujiajiri ndio unahitajika.
Nguli ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha inawezesha mazingira bora na rafiki kwa vijana wabunifu kwa kutoa mikopo, ajira na kuwapa fursa mbalimbali kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akiwataka vijana kutumia taaluma vyema katika kung’amua fursa katika jamii.
“Leo limefanyika tukio kubwa katika historia, sisi kama Serikali nichukue nafasi hii kuwahidi wasomi kuwa watapata ushirikiano wa kutosha, tunafursa nyingi Serikalini, niseme dunia imebadilika, mazingira yamebadilika, tunafundishwa ili taaluma zetu tukazitumie katika maisha ya kawaida, nawaomba sana vijana tuwaze nje ya box kwa kuwa na mawazo ya ubunifu na sisi kama Serikali tutaunga mkono mawazo hayo,” amesema Nguli.