Ahmed Sagaff – Maelezo.
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Suleiman Jafo amesema kero nne zilizobakia katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaofikisha miaka 60 zinaendelea kupatiwa ufumbuzi na kwamba jitihada za utatuzi zimeimarika katika uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Jafo amezitaja kero hizo kuwa ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi ha Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.
Nyingine ni mgawanyo wa faida kutoka Benki Kuu, na uingizwaji wa sukari inayozalishwa katika kiwanda cha Mahonda katika soko la Tanzania Bara.
“Ufanisi umekuwa mkubwa sana. Nilitoa takwimu hapo mwanzo kwamba kipindi hiki tumeweza kutatua takribani kero 15 za muungano. Hili si jambo dogo kwa kipindi cha miaka mitatu kuweza kufanikisha,” amearifu Dkt. Jafo.
Naye, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amefahamisha kuwa Watanzania wanajivunia historia ya Taifa lao katika miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa Aprili 26, 1994.
“Natoa wito kwa waandishi wa habari na kuwaomba ushirikiano wenu katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano,” ameomba Matinyi.