Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Denis Kitambi amesema atazitumia mechi tisa zilizobaki kuiweka timu hiyo sehemu salama kwenye msimamno wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Kitambi amesema hiyo ni kutokana na kutumia mapumziko ya wiki mbili ya ligi kuimarisha upungufu wa kikosi chake uliosababisha kupoteza mechi kadhaa.

“Mechi zote tisa zilizobaki tumezipa hadhi ya fainali, malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda ili kujiondoa kwenye nafasi mbaya tuliyopo hivi sasa na hilo linawezekana sababu kitu kizuri ni kwamba mechi zote dhidi ya timu kubwa tumeshamalizana nazo,” amesema

Amesema kinachompa matumaini na uhakika wa kushinda mechi hizo ni kuimarika kwa kikosi chake baada ya kurekebisha makosa madogo madogo ambayo yalikuwa yakijirudia mara kwa mara kabla ya ligi haijasimama.

Pia amesema kila mchezaji amempangia jukumu lake la kufanya katika kila mechi watakayocheza na masharti yake ni kuhakikisha anatimiza kwa asilimia 75 kwenda juu akiamini hiyo ni moja ya mbinu itakayowasaidia kupata ushindi.

Geita Gold FC ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo ikivuna pointi 21 katika idadi kama hiyo ya mechi na Kitambi amesema hayupo tayari kuona timu hiyo inashuka daraja.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 27, 2024
Dkt. Jafo: Kero za Muungano zinakaribia kumalizika