Mkuu wa msafara wa Al Ahly, Hossam Ghally, amesemna kizuizi kikubwa kwao kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC ni uwepo wa Kocha Abdelhak Benchikha.
Al Ahly inatarajiwa kuvaana na Simba SC keshokutwa Ijumaa (Machi 29) kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza timu hizo zinakutana kwenye hatua hiyo.
Simba SC ilirejea jijini Dar es salaam jana Jumanne (Machi 26) ikitokea Visiwani Zanzibar ilipokuwa imeweka kambi ya juma moja, huku wachezaji wa Al Ahly wakitarajiwa kuwasili nchini leo Jumatano (Machi 27).
Ghally ambaye ni kiungo wa zamani Al Ahly, amesema Simba SC ni timu bora kwani wamekutana nayo mara kadhaa, lakini sasa wana wasiwasi zaidi kwa kuwa ipo chini ya kocha mzoefu Barani Afrika.
Ghally aliyetwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika akiwa na Misri mwaka 2010 ni kati ya viongozi wa heshima wa klabu hiyo akiwa ametumwa hapa nchini ili kuhakikisha timu hiyo inafikia sehemu salama.
Amesema mechi yao ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa itakuwa ngumu kutokana na rekodi ya Benchikha ambaye kila walipokutana naye amekuwa akiwapa wakati mgumu.
“Simba SC tunaweza kuifunga, Lakini nadhani kitu kinachotufanya tuwe na wasiwasi ni uwepo wa Kocha Benchikha (Abdelhak), nadhani mnafahamu ubora wake kwa sasa na namna anavyojua kusimama na mbinu zake,” amesema
“Nipo hapa kuhakikisha timu inapata wakati mzuri wa mechi hii ya Ijumaa (Machi 29), tunaamini makocha wetu watakuja na mpango mzuri wa kupata matokeo mazuri, hatujawahi kupata ushindi hapa Kwa Mkapa tukicheza na Simba SC, hili ni eneo lingine ambalo linatufanya tuwe makini na mechi hii.
“Sina wasiwasi na kikosi chetu tutacheza kwa ubora wetu kupata matokeo mazuri ambayo yatatupa wepesi kabla ya mechi ya marudiano kule Cairo, tunataka kutetea ubingwa wetu msimu huu,” amesema Ghally aliyewahi kuitumikia Tottenham Hotspur ya England.
Benchikha anasifika kwa kusimamia ajenda moja mpaka mwisho wa msimu akiwa amewahi kufanya hivyo akiwa na RS Berkane ya Morocco na USM Alger ya Algeria, kisha zote akazipa makombe ya Shirikisho Afrika.
Mechi yake ya mwisho kukutana na Ahly ilikuwa ile ya mwaka jana ya Super Cup, ambapo timu yake ya USM ilibuka na ushindi wa bao l-0 na kuchukua ubingwa.
Simba SC na Ahly zimekutana mara nane, kila moja imeshinda nyumbani kwake michezo mitatu zikitoka sare kwenye mechi mbili, mmoja Dar es salaam na mwingine Cairo Misri, kwenye mechi hizo Ahly imefunga mabao 12, huku Simba SC ikifunga saba.