Rais wa zamani wa Chama cha Soka cha China (CFA), Chen Xuyuan amefungwa maisha baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na rushwa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo, Januari mwaka huu rais huyo alikiri kupokea rushwa ya Yuan milioni 81 sawa na dola za Marekani Milioni 11.2 au Pauni Milioni 8.9 za Uingereza.
Tume ya kupambana na rushwa iliyoongozwa na rais Xi Jinping inapambana na kadhia hiyo kwenye michezo, benki na jeshini.
Kwenye soka makocha na wachezaji mbalimbali wanaendelea kuchunguzwa kujihusisha na rushwa.
Mahakama ya Huangshi ilifichua Chen kujihusisha na kazi zilizo kinyume na sheria kutoka mwaka 2010 na 2023, ambayo ilijumuisha shughuli zake za awali kama rais na mwenyekiti wa kampuni ya International Port Group.
Waendesha mashtaka walisema Chen alikubali kuchukua fedha na vitu vya thamani kubadilishana na msaada anaoweza kutoa wa kuingia mikataba mbalimbali na kuandaa matukio ya michezo.
Mahakama ilisema Chen amefanya uharibifu mkubwa kwenye soka la China kwa mujibu wa Shirika la Habari linalomilikiwa na serikali ya nchi hiyo la Xínhua.
Shirika hilo la habari pia lilisema maofisa wengine watatu wa juu kwenye chama cha soka cha China pia walihukumiwa kwenda jela kwa miaka kati ya minane na 14 kwa rushwa.
Mapema mwaka huu, kiungo wa zamani wa Everton na timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Chína, Li Tie, alikiri kupanga matokeo na kutoa rushwa kwa watu akiwemo Chen kupata kazi ya ukocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo.