Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Brazil, Vinicius Jr amesema anahisi kama hana hamu ya kucheza soka kwa sababu ya unyanyasaji wa mara kwa mara wa kibaguzi aliofanyiwa.
Msimu uliopita kulikuwa na matukio 10 ya aina hiyo dhidi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, yaliyoripotiwa kwa waendesha mashtaka na La Liga.
Wakati wa mkutano wa waandishi wa habari, Vinicius alisema kuwa hataondoka Real Madrid na Hispania, kwani kwa kufanya hivyo ataruhusu ubaguzi wa rangi kushinda.
Hata hivyo, alisema alikuwa anaona ni vigumu kusonga mbele kutokana na unyanyasaji huo.
Brazil jana Jumanne (Machi 26) ilicheza na Hispania katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid kama sehemu ya kampeni ya kupinga ubaguzi wa rangi chini ya kaulimbiu ‘Ngozi Moja’.
Vinicius alisema: “Hakuniingia akilini kuondoka Hispania kwa sababu nikiondoka nitawapa wabaguzi kile wanachotaka.
“Nitabaki kwa sababu kwa njia hiyo wabaguzi wa rangi wanaweza kuendelea kuniona usoni zaidi na zaidi.
“Mimi ni mchezaji shupavu, nacheza Real Madrid na tunashinda mataji mengi na hilo haliwafurahishi watu wengi.
“Nataka tu kucheza soka, lakini ni vigumu kusonga mbele, najihisi kutopenda kucheza.”