Pamoja na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Timu ya Taifa ya Mongolia juzi Jumatatu (Machi 25), mechi iliyochezwa Uwanja wa Dalga Arena nchini Azerbaijan, Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman Marocco, amesema bado ana kazi ya kufanya kuinoa safu ya ushambuliaji kwani katika mchezo huo ilionekana kukosa mabao mengi ya wazi.
Kocha Morocco amesema nafasi nyingi zilizokuwa zinapatikana na kupotezwa, wakati mwingine hupatikana chache katika michezo mingine ya mashindano makubwa, hivyo inabidi zitumiwe vema.
“Kwa mimi, lakini bado nina kazi ya kufanya, kwa sababu tumetengeneza nafasi nyingi, ilikuwa tufunge mabao zaidi ya hayo, katika baadhi ya mechi za mashindano makubwa nafasi zile unazipoteza inakuwa shida, lakini pia huwezi kupata nafasi nyingi kama zile, utapata chache na unatakiwa kuzitumia, nafikiri tunapanda kidogo kidogo, lakini pia tuna kazi ya kufanya,” amesema kocha huyo.
Amesema baada ya mashindano maalum ya FIFA Series 2024, atakuwa na kazi ya kurekebisha hali hiyo katika michezo inayofuata huko mbele.
Akiizungumzia mechi hiyo, kocha huyo amesema kipindi cha kwanza hali ilikuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao walipaki basi, lakini kipindi cha pili walibadilisha mfumo na kuweza kupata idadi hiyo ya mabao ambayo kwake anasema yalikuwa ni machache kuliko nafasi zilizopatikana.