Wakati Simba SC na Young Africans zikiendelea kuchora ramani ya kuwamaliza wapinzani wao kwenye michezo ya Robo Fainali Ligi ya Bingwa Barani Afrika, nyota wa zamani wa timu hizo, Willy Martin ‘Garikubwa’ amewapa maujanja ya kumaliza kazi mapema.
Simba SC na Young Africans ndizo zinawakilisha Tanzania katika michuano hiyo zikiweka rekodi msimu huu ya kuwa nchi pekee ambayo imeingiza timu mbili kwenye hatua ya makundi.
Simba SC ambayo ni msimu wa nne mfululizo kutinga hatua hiyo watawakaribisha Al Ahly, mchezo ukipigwa keshokutwa Ijumaa (Machi 29), huku Young Africans wao wakiwavaa Mamelodi Sundowns Jumamosi (Machi 30), mechi zote zikipigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam.
Garikubwa amesema pamoja na ugumu wa mechi hizo, lakini anayo matumaini kwa wawakilishi hao wa Tanzania kufanya vizuri huku akiwapa siri namna ya kuvuka hatua hiyo.
Amesema Simba SC na Young Africans zina vikosi bora vya kuweza kuamua matokeo, hivyo wanapaswa kupambana kupata mabao ya mapema ili kuwatoa mchezoni wapinzani, lakini kutokubali kuchezea mipira eneo la hatari.
“Uhakika timu hizo zitashinda, lakini lazima wapambane kupata mabao ya haraka, idadi iwe zaidi ya mawili lakini wajiamini wanapokuwa uwanjani kwani wapo nyumbani,” amesema Garikubwa.
Nahodha huyo wa timu hizo aliwataka Henock Inonga, Che Malone (Simba SC), Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Dickson Job (Young Africans) kuwa makini kutokana na timu pinzani kuwa na mpira wa mashambulizi muda mwingi na hivyo wahakikishe hawakai sana na mpira langoni kwao.