Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma inatarajia kuanzisha ushirikiano wa matibabu na Hospitali ya Rufaa ya Mjini Magharibi (Lumumba), Zanzibar katika huduma za kibingwa, unaolenga kubadilishana uzoefu.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh wakati akipongeza ujio wa Viongozi wa BMH ulipomtembelea ofisini kwake na kusema Hospitali ya Lumumba itanufaika kwa kubadilishana uzoefu.

Amesema, “nimefika Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma nikajionea utayari wa Madaktari Bingwa na Vifaa vya kisasa mnavyovitumia, nimefika kwenye wodi maalumu ya Uloto nikiri kwamba naona fahari kuja kwenu hapa maana yapo mengi tutakayo chukua kupitia ushirikiano huu.”

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bi. Prisca Lwangili, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, amesema “Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa kwa kasi na kutoa matibabu ambayo hayapatikani Afrika Mashariki na Kati. Hivyo tumeona ni muhimu kusogeza huduma hizi hapa Zanzibar kwa kuwa hapa pia kuna uhitaji wa huduma za Upandikizaji Uloto ili kutibu seli mundu.”

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa BMH, Bi. Monica Kessy, uhusiano huu ni sehemu ya wajibu wa BMH ili kubadilishana uzoefu kati ya hospitali za umma huku, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji BMH, Dkt. Januarius Hinju, ameeleza utayari kwa Madaktari Bingwa wa BMH katika huduma.

Michael Olise aishughulisha Man Utd
Simba SC, Young Africans zapewa ujanja kimataifa