Mwana Fa apongeza shirikisho la IFPI kuchagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wao
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ameupongeza uongozi wa Shirikisho la Kimataifa la Watayarishaji wa Muziki Duniani (IFPI) kwa kuchagua Tanzania kufanya mkutano wao mkuu.
Mhe. Mwinjuma ametoa pongezi hizo Machi 26, 2024 Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano huo ambapo amesema, uamuzi huo ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa hakimiliki hapa nchini.
“Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan yamefanyika mageuzi makubwa, ikiwemo mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kwa lengo la kuhakikisha Wasanii wananufaika na kazi zao na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) wamefanya jitihada mbalimbali za kuimarisha mahusiano ya Kimataifa katika usimamizi wa hakimiliki,” amesema Mhe. Mwinjuma.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Bi. Doreen Anthony Sinare amesema mkutano huo, umelenga kuweka msisitizo wa viwango vya makusanyo ya mirabaha katika Redio na Televisheni kwa kuhakikisha wanalipia matumizi ya kazi za muziki na kuwa na makubaliano ya viwango vya makusanyo ambavyo havitofautiani sana.
“IFPI ni Shirikisho linalojihusisha na kusimamia haki za Watayarishaji wa Muziki na wamekuwa na utaratibu wa kuendesha mikutano yao katika nchi mbalimbali na hivi karibuni COSOTA tuliwaalika kufanya mkutano Mkuu wao Tanzania na waliridhia, kwa mkutano huu kufanyika nchini kutakuwepo na manufaa mengi kwa Watayarishaji wa muziki nchini pamoja na kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa hakimiliki kutoka nchi mbalimbali,” amesema Doreen.
Aidha, Bi. Doreen amebainisha kuwa hivi sasa nchi nyingi za Bara la Afrika zimekuwa zinapewa ushirikiano na viongozi wa kisiasa katika kuimarisha usimamizi wa hakimiliki ikiwemo Tanzania hivyo wamesisitiza kutumia fursa hiyo.
Naye Mratibu wa Mkutano huo kutoka IFPI Bi. Angela Ndambuki ameipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano huo na kueleza kuwa, kufanyika kwa mkutano huo nchini kutasaidia kuendelea kutangaza Muziki wa Tanzania katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na kufungua fursa mbalimbali kwa Watayarishaji wa Muziki wa Tanzania pamoja na Wasanii.