Sakata la Mshambuliaji Prince Dube juu ya mustakabali wake katika kikosi cha Azam FC limezidi kupamba moto, kufuatia klabu ya Young Africans kudaiwa kutuma ofa ya Sh. Milioni 521 kuinasa saini ya Mzimbabwe huyo.
Dube mwenye umri wa miaka 27, yupo nje ya kikosi cha Azam FC hivi sasa baada ya kuiandikia barua klabu hiyo kutaka kuvunja timu nyingine.
Hata hivyo, pamoja na Mshambuliaji huyo kupeleka Sh. Milioni 200 ili kumalizana na waajiri wake hao, Azam FC ilimtaka afuate mkataba unavyotaka ili avunje mkataba, ambapo ilidaiwa ili aachiwe huru anatakiwa kulipa dola za Marekani 300,000 (zaidi ya sh. milioni 700).
Pamoja na Azam FC kupokea ofa ya klabu za Simba SC na Al Hilal ya Sudan juu ya saini ya nyota huyo, imeelezwa kuwa vigogo wa Young Africans wamejiunga katika vita hiyo kutaka kukamilisha saini ya mchezaji huyo kutua katika mitaa ya Twiga na Jangwani.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Azam FC, tayari Yanga imeshatuma ofa ya Milioni 521 kuinasa saini mfumania nyavu huyo aliyepachika mabao saba katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Taarifa hizo za kuaminika zimedokeza kuwa, kama Young Africans itakubaliwa ombi hilo italipa fedha hizo kwa awamu Awali, Azam FC ilitangaza kuwa ipo tayari kumuuza Mzimbabwe huyo kwa klabu yoyote ndani na nje ya nchi kama tu itaafikiana nayo katika mazungumzo.
Afisa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zacharia ‘Zaka Zakazi’ amesema bado uongozi wa klabu hiyo haujampa taarifa rasmi kuhusu ofa hiyo.
“Sina taarifa mpya zaidi ya ile ambayo niliitoa awali, ni klabu mbili tu zilizoleta maombi ya kumtaka Dube, kama kuna zingine zinaweza kuja tu bado milango iko wazi,” amesema.
Ofisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amethibitisha kweli wametuma ofa hiyo, lakini kwa sasa ni mapema kuzungumzia hilo, na badala yake akili zao wamezielekeza katika mchezo wao wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, utakaopigwa Jumamosi (Machi 29) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Kamwe alisema baada ya kumaliza kibarua hicho ndipo watakuwa na nafasi kuzungumzia mambo mengine yanayohusiana na klabu yao.
Dube aliyetua Azam FC mwaka 2020 akitokea The Highlanders ya nchini New Zealand, anatarajiwa kumaliza mkataba wake katika klabu hiyo mwaka 2026.
Kama Mzimbabwe huyo atatua Young Africans katika dirisha lijalo la usajili, pengine timu hiyo ya wananchi inaweza kuacha baadhi ya washambuliaji wake wa kati akiwemo Kennedy Musonda, Clement Mzize na Joseph Guede.