Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema kurejea kikosini kwa walinzi Abdallah Sebo na Daniel Amoah kumeongeza uimara kwenye safu yake ya ulinzi.

Nyota hao wawili walikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu wakiuguza majeraha, Sebo alifanyiwa upasuaji mdogo wa goti wakati Amoah alikuwa akisumbuliwa na kifundo cha mguu.

Akizungumza jijini Dar es salaam kocha huyo amesema kurejea kwa wawili hao kutaongeza ubora kwenye safu yake ya ulinzi na kumfanya awe na nafasi pana ya kuchagua katika mechi zilizo mbele yao.

“Wamekuja wakati muafaka ambao tunahitaji kuwa bora ili kupata ushindi utakaotuweka karibu na malengo yetu ambayo ni ubingwa msimu huu,” amesema Dabo.

Kocha huyo raia wa Senegal amesema wachezaji hao wana uzoefu mkubwa na ligi ya Tanzania Bara, hivyo mchango wao katika kipindi hiki ni muhimu sababu hawapo tayari kuona wanapoteza mchezo kutokana na malengo waliyokuwa nayo msimu huu.

Amesema anatambua ushindani uliopo kwenye ligi na timu yake imeruhusu mabao 16 msimu huu lakini watapambana kuhakikisha wanacheza kwa tahadhari ili kuhakikisha hawadondoshi pointi katika mechi hizo tisa zilizobaki.

Azam FC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikikusanya pointi 45 katika michezo 21 huku mabingwa watetezi Young Africans wakiwa kileleni na pointi 52 na michezo 20.

Azam FC yaikana ofa ya Young Africans
Rulani Mokwena aishtukia Young Africans