Beki wa kulia wa Simba SC, Shomari Kapombe ameitabiria ushindi mnono timu yake katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.
Beki huyo amesema kwa maandalizi wanayofanya ana matumaini makubwa na ushindi katika mchezo huo utakaochezwa keshokutwa Ijumaa (Machi 29) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
“Maandalizi yetu yanakwenda vizuri kila mchezaji amekuwa akijituma zaidi kwa lengo la kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo wetu wa keshokutwa Ijumaa (Machi 29), najua haitakuwa kazi rahisi lakini dhamira yetu na ushindi ukizingatia tutakuwa nyumbani,” amesema Kapombe
Beki huyo amesema kinachowapa jeuri ni kuwafahamu vizuri wapinzani wao Al Ahly kutokana na kukutana nao mara nyingi zaidi siku za karibuni lakini pia kikosi chao kimeimarika zaidi kwa kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa na mashindano hayo.
Amesema kambini kwao kila mchezaji ameonesha utayari wa kuitaka mechi hiyo, hivyo inampa matumaini ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo ambao umebeba hatima ya kufikia malengo waliyojiwekea msimu huu ya kucheza hatua ya Nusu Fainali kwenye michuano hiyo.
Kapombe ni miongoni mwa wachezaji wazoefu wenye kikosi cha Simba SC, ambacho kina rekodi ya kucheza Robo Fainali nne kwenye michuano hiyo kwenye misimu iliyopita.