Baada ya kurejea jijini Dar es salaam ikitokea Zanzibar ilikokuwa imeweka kambi, Simba SC imebeba siri nzito kuelekea mchezo wake wa mkondo wa kwanza wa Robo Fainali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa keshokutwa Ijumaa (Machi 29), Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Kuelekea mchezo huo Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Selemani Matola amesema kambi ya Zanzibar imewaimarisha kwa kiasi kikubwa na imewaongezea wachezaji wao ari ya kupambana kupata ushindi katika mchezo huo aliosema wanaupa uzito mkubwa.

“Tumerejea tukiwa na nguvu mpya kitu kizuri ni kwamba tumefikia kambini kwa ajili ya kuongeza vitu viwili vitatu kwa wachezaji wetu ambao wameahidi kupambana kufa au kupona kwa ajili ya kuipa Simba SC ushindi kwenye ardhi ya nyumbani,” amesema Matola.

“Tunatambua mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na wapinzani wetu kukutana nao mara nyingi, lakini silaha kubwa tunayojivunia nayo kuelekea kwenye mchezo huo ni uwepo wa Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha kwenye Benchi letu la ufundi.”

“Benchikha anewajua vyema wapinzani wetu ikiwemo mbinu zao chafu zinazowapa ushindi, hivyo katika maandalizi yetu amewapa wachezaji silaha muhimu ambazo kama wachezaji wakizitumia ipasavyo ninaamini tutavuna ushindi mnono tukiwa nyumbani.”

“Tunachohitaji ni kuumaliza mchezo huu tukiwa kwenye ardhi ya nyumbani na kwa maandalizi tuliyofanya na utayari waliokuwa nao wachezaji,  ninaamini tutakuwa na asilimia kubwa ya kupata ushindi.” amesema Matola

Katika hatua nyingine Matola amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kuipa sapoti timu yao na kutengeneza rekodi ya pili kwa kumtoa bingwa mtetezi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, rekodi ya kwanza waliiweka mwaka 2003 kwa kuitoa Zamaleki pia ya Misri katika hatua ya kuingia makundi.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 28, 2024
Shomari Kapombe: Tutapambana hadi kieleweke