Kupitia ukurasa wao wa mtandao wa Kijamii, Mabalozi wa Usalama Barabarani – RSA, wamebainisha mojawapo ya chanzo cha ajali za barabarani na hata zile za anga, reli, na majini kuwa zinatokana na tabia ya binadamu au kama inavyofahamika na wengi kuwa ni makosa ya kibinadamu.

RSA inasema “mojawapo ya makosa hayo, ni dereva au kwa lugha ya kimombo “driver error” ambapo kule kwenye ndege na majini huitwa “pilot error”. Kwenye ndege makosa ya rubani yametajwa kuchangia 78.6 ya ajali zote za ndege. Sasa je, “driver error” ni nini? Na je ni wakati gani tunapoweza kufikia hitimisho la kusema chanzo kikuu cha ajali hii ni kosa la dereva.”

Andiko hilo linaendelea kufundisha kuwa, ajali inayotokana na makosa ya dereva ni ile ambayo tendo au uamuzi uliofanywa na dereva katika kuliendesha gari kuwa chanzo kikuu cha ajali, ikihusisha dereva kushindwa kufanya maamuzi sahihi au kuchukua hatua sahihi barabarani (dereva kukosea hesabu), mathalani wakati wa kuovateki.

Wanasema, “unaweza kuta gari ni zima kabisa halina tatizo na barabara haina tatizo lakini bado dereva akapata ajali kutokana na hicho kinachoitwa “driver error”. Baadhi ya maamuzi hayo yanaweza kuwa kuongeza mwendo, kulipita gari jingine, kulisogelea gari jingine kwa karibu sana kwa nyuma (tailgating), kuamua kusimamisha gari kwenye kona bila tahadhari, nk.

RSA wanaongeza kuwa, wakati mwingine makosa ya dereva huweza kusababishwa na gari lenyewe kwenda vibaya, sasa uamuzi ambao dereva anauchukua baada ya pale ndio hupelekea ajali. Kwa mfano, tairi moja la gari limepasuka. Maamuzi atakayoyachukua dereva kama mwitikio (reaction) ya kupasuka kwa tairi yanaweza kuamua iwe ajali au isiwe.

Mara nyingi gari inaweza kuwa katika mwendo mkubwa au wa wastani, na ghafla dereva akakutana na shimo au kona, maamuzi atakayoyafanya pale yanaweza kusababisha ajali. Vivyo hivyo, anapokuwa anahisia gari linatoka nje ya barabara, ambapo makosa hayo, huwa siyo matendo ya bahati mbaya, bali ni matendo ya kukusudia ambayo huwa hayaleti matokeo yaliyotarajiwa.

Kwa kufanya matendo au kuchukua maamuzi hayo, dereva anakuwa hanuii ajali. Lengo lake linaweza kuwa zuri la kuepusha ajali au kumkwepa mtu mwingine, lakini katika kufanya hivyo akapata ajali. Iwapo kama maamuzi hayo yangeenda kama alivyopanga basi matokeo yake yasingekuwa ajali.

Makosa ya dereva, pia yanahusishwa na matatizo ya kisaikolojia au kifiziolojia anayoyapata dereva akiwa kazini. Yale ya kisaikolojia yanahusisha msongo wa mawazo, furaha iliyopindukia, au hasira, wakati yale yanayohusu fiziolojia yanahusu namna viungo au mwili wa binadamu unavyoitikia vichocheo mbalimbali au kufanya kazi.

Wametoa mfano, mguu kupata ganzi, usingizi au kushikwa na msuli wakati dereva akiendesha gari, huku sababu nyingine ikiwa ni uchovu, ugonjwa, matumizi ya madawa ya kulevya, msongamano wa kazi, hofu, mawasiliano mabaya kati ya dereva na mtu mwingine (poor inter-personal communications), na kuchelewa kwa ubongo kuchakata taarifa, na kuruhusu viungo vifanye maamuzi.

“Ndio utaona kwa mfano ajali inataka kutokea mtu ameduwaa tu hadi anagongwa au dereva anahisi amekanyaga breki kumbe ameegesha mguu tu. Dereva pia anaweza kukoseshwa na vipimo au taarifa za gari lake mwenyewe. Mfano, speedomita inamwambia yupo spidi 50 wakati kiuhalisia yupo 80,” wameandika RSA.

Hata hivyo, vitisho vinatajwa kuwa ni moja ya vitu vinavyoweza kuchochea dereva kufanya makosa. Mfano, dereva akiwa barabarani anatishiwa kupigwa au kuuawa na watu, au anatishiwa kufutwa kazi au anaambiwa akifika mahali fulani atakamatwa na kuwekwa mahabusu.

Sababi hizi zinatajwa kuwa ni sbabu kwa dereva mwingine kuweza kufanya makosa yanayoweza kumsababishia ajali. Vitisho vinaweza vikawa ni vya kimazingira (mfano. Hali mbaya ya hewa, radi, mteremko mkali au kona, uwingi wa magari barabarani nk) au vya kiudereva, ambayo kwa kiasi kikubwa uongozi wa dereva unaweza kuvishughulikia.

Kwa ufupi, RSA wanasema yapo masuala mengi yanayoweza kuchochea au kushawishi mwenendo au maamuzi ya dereva barabarani. Haya yote yanatakiwa kuzingatiwa na wachunguzi wa ajali (crash investigators) kabla ya kufikia hitimisho la chanzo cha ajali.

Ndio maana mara nyingi ajali huchunguzwa kwa kuangalia mtiririko wa matukio (chain of events), kama ambayo nadharia za James Reasons (Swiss cheese model of causation) na wana imani kuwa kupitia andiko hili utakuwa umeongeza maarifa kuhusu makosa ya dereva kama chanzo cha ajali katika kundi la makosa ya binadamu kama kisababisha cha ajali.

RSA wanamalizia kwa kusema, “Usalama Barabarani ni Jukumu letu sote”, hivyo kama kila mtu atawajibika katika nafasi yake ni wazi kuwa haya mambo ya ‘Bosi kuna picha nimekurushia’ yatapungua na kutoweka kabisa.

Ripoti ya CAG: Deni la Taifa lafikia Trilioni 82
Mradi uboreshaji milki ardhi Nzega mbioni kukamilika