Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika Halmashauri ya Mji Nzega Mkoani Tabora umetekelezwa kwa asilimia 55 na kutarajiwa kukamilika Juni 30, 2024 ukiwa umetengewa Shilingi bilioni 1.42 ambapo kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 1.396 zilitengwa kwa ajili ya urasimishaji wa makazi na Shilingi milioni 24.926 kwa ajili ya kusimika alama za msingi za upimaji.

Akimkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga na ujumbe wake wakati wa ziara ya Kamati, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda amesema utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika mji wa Nzega unatekelezwa katika mitaa 14 iliyopo Kata za Nzega Mashariki, Nzega Magharibi, Nzega ndogo, Kitangiri na Uchama.

Amesema, katika kata ya Nzega Mjini Mashariki mradi unatekelezwa Mitaa ya Maporomoko, Uwanja wa Ndege, Msoma, Mwaisela, Nyasa pamoja na Kitongo. Aidha, Kata ya Nzega Mjini Magharibi mradi unatekelezwa katika mitaa ya Ipilili, Mbugani, Ushirika na Utemini na kwa upande wa Kata ya Nzega ndogo mradi unatekelezwa kwenye mtaa wa Zogolo. Kata ya uchama mradi unatekelezwa katika Mtaa wa Uchama na kwa kata ya Kitangiri Mradi unatekelezwa Mitaa ya Kitangiri na Budushi.

Awali, akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema katika halmashauri ya Mji wa Nzega mradi ulianza kutekelezwa Novemba, 2023 kwa lengo la kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 na kuongeza Alama za Msingi za Upimaji 14.

“Hadi sasa vipande vya ardhi 18,655 vimetambuliwa, vipande 8,814 vimepangwa na viwanja 3,960 vimepimwa na Alama za Msingi za Upimaji 14 zimesimikwa ardhini, kazi hii imetekelezwa kwa asilimia 55 na bado inaendelea na itakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa kwa kuwa sehemu kubwa kazi ambazo zinahitaji utaalam na muda mwingi zimeshakamilishwa,” alisema.

MAKALA: Bosi kuna picha nimekurushia
MALIMWENGU: Pande za mbili za Typhoid Mary - maradhi, vifo