Hatimeye Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limeutangaza Uwanja wa Tanzanite kuwa mwenyeji wa mchezo wa Fainali ya Kombe la Shiriksiho Tanzania Bara msimu huu 2023/24.
TFF ilikuwa kimya kwa muda mrefu kuhusu Uwanja ambao ulitarajiwa kucheza mchezo wa Fainali ya michuano hiyo msimu huu, ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao 2024/25.
Rais wa TFF Wallace Karia amesema Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo imekubaliana kwa pamoja kuwa, mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu, uchezwe katika Uwanja wa Tanzanite, ambao upo mjini Babati mkoani Manyara.
Amesema Uwanja huo umekidhi vigezo vyote vya kuwa mwenyeji wa mchezo huo, ambao kwa mara ya kwanza utakuwa mwenyeji wa mchezo wenye hadhi ya kitaifa.
“Kwenye kikao chetu kilichofanyika Babati mwezi uliopita tumeamua mchezo wa Fainali wa Kombe la Shirikisho utafanyika katika Uwanja wa Tanzanite, uliopo mjini Babati.”
“Huu ni Uwanja wenye viwango vizuri, umetengenezwa katika ubora mzuri, hivyo kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Manyara tunatangaza kuwa mchezo wa Fainali mwaka huu utachezwa hapo.”
“Tunatangaza hivi lakini watu wengi hawajui, lakini kila anayekwenda pale akifika atashangaa, kuna kitu kikubwa kimefanyika pale, kwa hiyo mchezo wa Fainali utachezwa katika Uwanja wa Tanzanite.” amesema Karia
Katika hatua nyingine Karia ametngaza rasmi kuwa michezo ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara mwaka huu, itachezwa katika viwanja viwili tofauti.
Amesema mchezo mmoja umepangwa kuchezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku Uwanja mwingine ukitarajiwa kutangazwa siku za usoni.
“Nusu Fainali zitakuwa mbili, moja tutacheza Mwanza, nyingine hatutangaza bado, hivyo nafasi bado ipo wazi kwa mkoa wowote ambao utakuwa umekidhi vigezo vya miundo mbinu, lakini pia vitu vingine ambavyo tutakuwa tumeviweka, kwa hiyo tutatangaza mkoa mwingine ambao utakuwa mwenyeji wa Nusu Fainali ya pili.”
“Kuna baadhi ya mikoa ambayo tumeipa changamoto hiyo ili waweze kurekebisha miundombinu ili tuweze kuwapa nafasi hiyo lakini bado tupo katika mchakato wa kuangalia utaratibu tuliojiwekea.”
“Hii ni sehemu ya mikakati wa wa kuhakikisha mpira unachezwa karibia nchi nzima. Kwa hiyo tumetoa nafasi kwa sehemu yoyote, na watendaji wa TFF wataendelea kufuatilia na watatueleza ni sehemu gani ambayo inakidhi.” amesema