Wataalamu katika Idara ya ENT ya Hospitali ya Benjamin Mkapa – BMH, wamefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto mdogo kwa siku sita.
Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo wa BMH, Emmerenceana Mahulu amesema BMH ilimpokea mtoto huyo wa miaka miwili siku ya Alhamisi ya Machi 26, 2024.
Amesema, “tumefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto kwa siku sita kwa kutumia kifaa tiba kinachoitwa esophagoscopy,” amesema Daktari huyo Bingwa ambaye pia Kaimu Mkuu wa Idara ya ENT ya BMH.
Dkt Mahulu amefafanua kuwa sehemu ya koo ilipokuwa imekwama sarafu ilisabisha uvimbe, akiongeza kuwa ilikuwa imeacha uwazi kidogo ambayo ilikuwa ikiruhusu vimiminika kama uji, maji juisi kupita na kwamba hali yake inaendelea vizuri baada ya matibabu na anaweza kula vizuri.
Kwa mujibu wa mama wa mtoto, Juliana Yuda ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mkoka kilichopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, amesema mtoto wake ambaye alitoka kucheza na wenzake siku ya Jumamosi Machi 20, 2024 na alirudi nyumbani muda wa mchana akiwa analia.
“Mtoto alikuwa hawezi kula kwa muda wa siku sita, alikuwa anashindia uji, juisi na maji tu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya Siku ya Alhamisi, na Alhamisi ya tarehe 26, Machi alimpeleka mtoto Hospitali ya Wilaya ya Kongwa ambapo alipewa rufaa kuja BMH baada ya kupigwa picha ya x-ray na kubaini sarafu imekwama kwenye koo,” alisimulia mama wa mtoto huyo.