Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inachukua kila jitihada kuhakikisha wafanyakazi nchini wanalindwa dhidi ya ajali, magonjwa na vifo katika shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Hayo yamesemwa katika hotuba yake ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025 aliyoiwasilisha Bungeni Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) imejipanga kuhamasisha na kusimamia usimikaji wa mifumo madhubuti ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi kwenye maeneo ya kazi nchini.
“Kwa mwaka 2024/2025 Serikali kupitia OSHA imepanga kufanya kaguzi 300,000 katika maeneo ya kazi 25,000, kupima afya za wafanyakazi 380,000 na kutoa mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi na wajasiriamali wapatao 38,000. Utekelezaji wa mpango huu unalenga kuendelea kusimamia Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ili kujikinga na athari za vihatarishi sehemu za kazi,” amesema Majaliwa.
Aidha, taarifa hiyo ya Waziri Mkuu imeonesha kuwa hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/2024 OSHA imefanya kaguzi maalum 187,093 sawa na asilimia 66.8 ya lengo la mwaka katika maeneo ya kazi 13,856 ikiwa ni pamoja na kuchunguza afya za wafanyakazi 253,691 na kutoa ushauri stahiki kutokana na matokeo ya uchunguzi huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Hassan Toufiq, wakati akisoma taarifa ya Kamati ya hiyo kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Pamoja na maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ameiomba Serikali kuiongezea bajeti OSHA ili kuiwezesha kutekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.