Chama cha Madaktari nchini Kenya – KMPDU, kimemtaka Rais William Ruto kuingilia kati mvutano unaoendelea kati yao na Wizara ya afya, ambao umekuwa ukitatiza huduma kwenye Hospitali za umma.

Uamuzi huo umekuja ikiwa tayari Serikali kusema itatimiza baadhi ya matakwa ya madaktari, ikiwa ni pamoja na kulipa malimbikizo na kuajiri madaktari wanafunzi kwa mikataba ya kudumu, miongoni mwa malalamiko makuu.

Hapo jana Aprili 4, 2024 Madaktari walikataa pendekezo la serikali linalolenga kumaliza mgomo wa wiki tatu, wakati mahakama ya kazi ikiweka tarehe ya mwisho kwa mzozo huo kutatuliwa.

Idadi yao inafikia Wanachama 7,000 wa muungano huo wa Chama cha Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa meno na walifanya maandamano katikati ya mwezi Machi kudai malipo bora na mazingira mazuri ya kazi.

Hata hivyo, Mahakama ya kazi jijini Nairobi ilisitisha mgomo huo mwezi uliopita na Aprili 3, 2024 iliamuru mazungumzo ya kumaliza mgomo huo yakamilike ndani ya siku 14.

Madaktari hao, wanataka kutekelezwa kwa mkataba wa maelewano wa mwaka 2017, uliolenga kuwaongezea mshahara, kuboreshewa mazingira ya kazi na kuajiriwa kwa Madaktari Wanafunzi.

Wakutana kujadili utekelezaji shughuli za EITI nchini
Usimamizi mifumo ya usalama mahala pa kazi waendelezwa