Bondia wa ngumi za kulipwa, Twaha Kassim ‘Kiduku’ amesema yupo vizuri kuanzia kiafya hadi mazoezi kuelekea katika pambano la ‘Hatukimbii Hatuogopi’ litakolofanyika Sikukuu ya Eid Pili, mkoani Morogoro.

Kiduku atashuka ulingoni kuzichapa na Harpreet Singh kutoka India katika pambano lisilo la ubingwa la raundi 10, uzito wa juu.

Akizungumza mjini Morogoro, Kiduku amewaomba mashabiki wake na wadau wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo, kuhakikisha wanapata burudani ya aina yake.

“Niko vizuri kuanzia kiafya kila kitu, mashabiki waje kwa wingi siku ya pambano, mimi sitowaangusha kwa sababu nimefanya programu za mazoezi mbalimbali,” amesema Kiduku.

Kiduku alieleza kuwa siku ya pambano hilo, Watanzania watapata burudani nzuri kutoka kwake kutokana na aina ya mazoezi anayoyafanya.

“Nitacheza kwa kiwango kizuri ambapo siku hiyo mashabiki zangu watafurahi, pia pambano litakuwa zuri kutokana na mpinzani ninayecheza naye,” amesema Kiduku.

Kocha wa bondia huyo, Pawa Iranda amesema anaendelea kumfua bondia wake awe na kiwango bora cha kumpiga Singh.

Iranda amesema maandalizi yanaendelea vyema na malengo yake ni kulitumia pambano hilo kurejesha makali ya bondia wake katika medani ya ngumi.

“Malengo yetu ni kurudisha heshima kwa mashabiki, wadau na Watanzania kiujumla, hivyo tutahakikisha pambano hili Kiduku anarekebisha makosa ya nyuma,” amesema Iranda.

Kiduku anapanda ulingoni akiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa pointi baada ya kupigwa na Asemahle Wellem wa Afrika Kusini, pambano lilofanyika Julai 29, mwaka jana.

Mkataba wa Kepa kusitishwa Real Madrid
FECAFOOT yakana ujio wa kocha mpya