Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohammed Abdallah ‘Bares’, amesema licha ya kukiandaa kikosi chake kimbinu, ametumia dakika 180 kuisoma Simba SC katika michezo ya Kimataifa.
Amesema amewaangalia mchezo wa mkondo wa kwanza na leo Ijumaa (Aprili 05) atawafuatilia Wekundi hao wa Msimbazi katika mechi ya marudiano ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly nchini Misri.
Hatua hiyo ni baada ya Mashujaa FC kuwakaribisha Simba SC Uwanja, wa Lake Tanganyika, Kigoma katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la CRDB Bank Aprili 9, mwaka huu.
Bares amesema wamejiandaa vizuri na wanawafahamu Simba SC, lakini amelazimika kutumia mechi mbili za kimataifa kuwaangalia kuona ubora na madhaifu yao kabla ya kukutana nao.
Amesema hatua ya kuwafatilia Simba SC kwa sababu ya ubora wao na kila mechi wamekuwa na mabadiliko hali inayomlazimu kuangalia kimbinu na kujipanga vilivyo katika mchezo wa hatua ya 16 ya Kombe la CRDB Bank.
“Tumekutana na Simba SC katika ligi hapa nyumbani na walitufunga, wako bora na hii michuano ya Kimataifa inazidi kuwafanya kuwa bora zaidi na kuendelea kujipanga vizuri kwa sababu wanacheza na timu bora Afrika, dhidi ya Al Ahly.” amesema Bares