Scolastica Msewa, Mkuranga – Pwani.
Mtoto Sharif Nuzran Almadar (13) ametoa sadaka ya iftar kwa watoto yatima 130 wa Mkuranga Mkoani Pwani na kuwaongoza kumfanyia Dua maalumu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kuongoza nchi kwa usalama na amani.
Watoto hao yatima ni kutoka katika mji wa Mkuranga ambao hawana kituo maalumu cha kuwalea na wenye mahitaji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nguo na vifaa mbalimbali vya shule na unifomu ikiwa ni pamoja na miongozo ya dini.
Iftari hiyo imefanyika mjini Mkuranga na pia kuhudhuriwa na ndugu na jamaa, majirani zao na viongozi mbalimbali wa serikali wilayani Mkuranga akiwemo Mwenyekiti wa halmashauri ya Mkuranga Mohamed Mwela.
Nuzran maarufu kama Shehe Sharif Nuzran amesema dua hiyo mbali na kumuombea kumuombea Rais Samia, pia inamuhusu Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasiri Ally na viongozi wengine wa Chama na Serikali.
Mama Mzazi wa Shehe mtoto Sharif Nuzran Almadar ambaye ni Diwani Viti maalum jimbo la Mkuranga, Bi Mariam Masaninga amewataka wazazi kulea watoto wao katika misingi ya dini na kutoa ushirikiano kwa watoto wao kutimiza ndoto zao katika maisha.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga na Diwani wa Kata ya Mkuranga Mohamed Mwela amewapongeza mama mzazi wa Shehe mtoto Sharif Nuzran Almadar na kwa sadaka waliyotoa kwa watoto hao yatima na kutenga muda wao kufanya Dua kwa viongozi wa Chama na serikali.
Babu wa Shehe mtoto Sharif Nuzran Almadar ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mkamba Hassani Dunda amesema amemuelewa mtoto huyo muda mrefu sana alipoanza kufanya ibada za masuala ya uislamu sasa ni mwaka wanne mfululizo.
Dunda amesema kufutulisha watoto yatima ni jambo kubwa alilofanya mtoto huyo kwani hata wao watuwazima wamejifunza kitu kutoka kwake kwani wao hawajawahi kufanya jambo kama hilo.
Imamu wa Msikiti wa Kivule ambaye ndio miongoni mwa watu wanaomlea Shehe mtoto Sharif Nuzran Almadar amsema kufutulisha watoto yatima ni jambo kubwa sana kwa mwenyezi Mungu na thawabu yake pia mbele za Mungu ni kubwa sana na ameitaka jamii kwa ujumla kuendelea kuwakumbuka kwa hali na mali watoto yatima.