Timu ya Madaktari bingwa 18 wakiwemo wauguzi na wataalam wa usingizi kutoka nchini Marekani wamewasili leo Aprili 6 mkoani Katavi kwa ajili ya kambi maalum ya kutoa huduma ya upasuaji wa kibingwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mpanda, mkuu wa msafara huo Profesa Eddie Chan amesema timu hiyo itatoa huduma ya upasuaji wa uso na kichwa (Craniofacial Surgery), upasuaji wa masikio, pua na koo (Otorynolaryngology Surgery) na upasuaji wa eneo la tumbo (General Surgery).

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Tanganyika, Dkt. Alex Mrema amesema ujio wa madaktari hao utawaodolea wananchi changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa kwani hadi sasa wagonjwa wanalazimika kupata rufaa kwenda Mbeya, Bugando, Benjamin Mkapa na Muhimbili kufuata huduma hizo jambo ambalo ni gharama kubwa.

“Wananchi wengi walikuwa wakishindwa kufikia huduma pale wanapopatiwa rufaa, hivyo madaktari hawa watakuwepo Wilaya ya Tanganyika kwa muda wa siku 7 kuanzia leo hadi tarehe 13 ambayo wataondoka kurudi Chicago,” amesema Dkt. Mrema.

Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wa Shirika la NORBERT & FRIENDS MISSIONS/OPERATIONAL INTERNATIONAL wameleta wataalam hao leo na huduma hizo zitaendelea bila malipo hadi April 13, 2024.

Mtoto atoa iftar kwa Watoto 130 kuliombea Taifa
Rais Samia hahusiki sadaka ya 5,000 Pemba ni upotoshaji: RC Amour