Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amewashauri Watanzania kuutumia mwezi mtukufu  wa Ramadhan kama jukwaa la kuwaelimisha Wananchi kudumisha upendo, umoja na maelewano.

Shaka ameyasema hayo leo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati wa mashindano ya kuhifadhi Quraani walioshirikisha washiriki kutoka mkoa wa Pwani na Iringa yaliofanyika katika viwanja vya Msikiti Bomani.

Amesema, siku zote  imani za dini zimekuwa zikitumika na kuwa kiungo kinachounganisha  watu, hivyo vibaki kuwa mwiko na marufu dini kutumika kuwagawa wananchi aidha kwa madhehebu zao, kanda au kwa makabila yao.

Shaka ameongeza kuwa kila Mtanzania na muumini wa dini  yake aelewe kuwa taifa halina dini bali  wananchi  wake ndiyo wenye kufuata imani  za dini na viongozi wa dini wanatakiwa kulisimamia hilo.

“Kila mtanzania nchi yetu inamtambua ni binadamu anayestahili heshima na haki kwa mujibu wa katiba  yetu. Taifa  letu  katiba yake imempa uhuru  wa kuabudu bila kuvunja mpaka, Kikitokea chama au kundi  chenye lengo la kuvuruga amani na kupandikiza chuki lilaaniwe na jamii ya watanzania,” amesema.

Aidha, Shaka aliwataka viongozi  wa dini  waendelee na kazi ya kuipika mioyo  ya waumini  wao  huku wakiwahimiza na kuwaeleimisha fadhila na neema za kumuamini Mungu ili waifanye mioyo yao iwe na rutuba ya upendo na kuwajali wenye dini na hata  wasio na dini.

“Nawahusia muufanye mwezi huu mtukufu  wa Ramadhan uwe jukwaa la uadilifu linalotoa elimu itakayowajengea maarifa  waumini  na wasio na dini .Viongozi wa dini zote waendelee kuhubiri upendo ndani na nje ya nyumba za ibada. Misikiti na makanisa yaendelee na kazi ya kuelimisha imani na umoja,” alisema.

Naye kadhi wa Mkoa wa Morogoro, Mohamed Masenga amesifu jitihada za viongozi wa serikali katika kuwaunganisha watanzania jambo ambalo nchi imeendelea kuwa na amani, upendo na umoja huku wakishuhudi mipango mbali mbali ya kuletea maendeleo ikifanikiwa.

Wawili wakamatwa wakisafirisha mifugo nje bila vibali
MALIMWENGU: Usikae chini kungoja mafanikio, nyanyuka