Gavana wa Baringo, Benjamin Cheboi na Mbunge wa Ainabkoi, Samuel Chepkonga wote wa Nchini Kenya, wameomba nguvu za Kiungu kupitia maombi zitumike, ili kumaliza mgomo wa madaktari unaoendelea, wakiwatahadharisha Madaktari kuwa Mungu atawaadhibu kwa kwenda kinyume na kiapo chao kutokana na kupenda pesa.
Wakizungumza katika eneobunge la Ainabkoi, Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa mazishi ya daktari wa mifugo Peter Kale, ambaye hadi kifo chake alikuwa Mhadhiri katika chuo cha mafunzo ya ufugaji Naivasha Dairy Training Institute ,kwa pamoja walionya kuwa Mungu atawaadhibu madaktari kwa kuzingatia zaidi pesa badala ya shida za wagonjwa.
“Nawasihi maaskofu na viongozi wengine wa kidini tuwaombee madaktari wetu Mungu awaguse wajue maisha ya binadamu ni muhimu kuliko fedha na tofauti zao na watu wengine. Pesa haitakupeleka mbinguni hata ukipata kiasi gani, ni hofu ya Mungu pekee ndiyo itakupeleka mbinguni,” alisema Cheboi.
Hata hivyo, alipongeza asilimia 70 ya Madaktari kutoka kaunti yake kwa kupuuza mgomo na badala yake kuendelea kuhudumia Wagonjwa, akisema Serikali inafanya kila iwezalo kutatua malalamishi yaliyotolewa na madaktari hivyo lazima wazingatie mahangaiko ya Wakenya.
Hata hivyo, Rais wa Kenya William Ruto alisema kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kuwalipa wafanyakazi nchini humo na kwamba Madaktari hao watalazimika kurudi kazini kutokana na ukweli kwamba hakuna pesa ya kuwapa kama wanavyotaka.