Watu watano wamefariki dunia jijini Blantyre nchini Malawi, huku wengine wawili wakipokea matibabu baada ya kudaiwa kunywa pombe ya kienyeji yenye sumu.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Afya na Huduma za Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Blantyre, Gift Kawalazira imethibitisha kutokea kwa vifo vya watu hao na kusema pombe hiyo ni ile ya bei nafuu inayotumiwa zaidi na vijana wasio na ajira na baadhi ya watoto wadogo.
Kufuatia vifo hivyo, Polisi imesema imeanza msako wa watengenezaji na wauzaji wa pombe ya kienyeji inayofahamika kwa majina mbalimbali ya yakiwemo “nichukue Bwana”, “stagger” na “monkey killer”.
Hata hivyo, Polisi pia imefahamisha kwamba hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mkasa huo na kwamba wataendelea kupambana na visa mbalimbali vinavyohusiana na unywaji wa pombe haramu.