Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA-ZNZ, kimewakumbusha Wazazi na Walezi kuendelea kuwalinda na kuhakikisha usalama wa watoto wao kueleekea katika sikukuu za Eid el Fitr.
Taarifa ya Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa iliyotolewa hii leo Aprili 9, 2024 imeeleza kuwa wanaungana na jamii katika sherehe hiyo ya kipekee lakini wanaikumbusha jamii kutosahau majukumu yetu katika kulinda na kuhakikisha usalama wa watoto.
“Hivi karibuni tumeendelea kushuhudia ongezeko la matukio ya udhalilishaji, kutoka matukio 1,360 mwaka 2022 hadi matukio 1,954 mwaka 2023, ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 43.7, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Mtakwimu Mkuu ambayo pia inaonesha kuwa waathirika wengi wa matukio haya ni watoto ambapo kwa mwaka 2023 walikua ni asilimia 83.7 ya waathirika wote,” ilieleza taarifa hiyo.
Kutokana na ripoti hiyo TAMWA-ZNZ imesisitiza umuhimu wa kuongeza jitihada katika kupunguza matukio hayo kwa kuwa karibu na kuzifuatilia nyenendo za Watoto/ Vijana kwa kipindi chote cha sherehe hizo, kwa kutambua pia umuhimu wa kulinda na kudumisha maadili hasa katika upande wa mavazi na mienendo kwa lengo la kuhakikisha usalama wa watoto.
“Kipindi hiki cha sikukuu ni fursa ya kipekee ya kuzingatia maadili haya na kuiweka jamii yetu katika mstari unaofaa. Tunatoa wito kwa kila mwanajamii kuchukua jukumu lake katika kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto wetu na jamii yetu kwa ujumla. Tunapoelekea kusherehekea Sikukuu ya Eid el Fitr, tunawatakia kila la kheri na furaha tele,” alisema Dkt. Mzuri kupitia taarifa hiyo.