Kiungo Mshambuliaji Young Africans Stephanie Aziz Ki amefichua alichozungumza na Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Afrika Kusini Mamelodi Sundowns Rhulani Mokwena, baada ya mchezo wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Young Africans ilicheza dhidi ya Mamelodi Sundowns Machi 30 katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza, kisha Aprili 05 kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili na timu hizo kupigiana mikwaju ya Penati na mshindi wa jumla kupatikana mjini Pretoria.

Aziz Ki alionekana kuwa mwiba dhidi ya Mamelodi Sundowns katika michezo yote miwili, hali ambayo imemfanywa kutajwa sana na Mashabiki wa soka wa Masandawana, na hata Benchi la Ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mokwena.

Hata hivyo ukimya ulitawala baada ya wawili hao kuonekana wakiteta baada ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza kupigwa jijini Dar es salaam, uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini Kiungo huyo kutoka Burkina Faso amefunguka kwa kuweka wazi alichoambiwa na Kocha Mokwena.

Aziz Ki amesema: “Kocha Rhulani Mokwena alinifuata na kuniambia wewe ni mchezaji mkubwa sana na una kila sifa. Una nguvu na una umiliki mzuri wa mpira miguuni mwako,akanishauri niongeze uharaka eneo la ushambuliaji ili kuwa bora zaidi. Amenisisitiza kufanya hivyo akiamini kuwa pia naweza na nitakuwa bora zaidi kwa kuwa na namba nzuri ya ufungaji na hili nitalifanyia kazi”

Aziz Ki alikaribia kuipeleka Young Africans Nusu Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kufuatia shuti lake kugonga mwamba wa juu na mpira kuangukia kwenye mstari, hali ambayo imeendelea kuleta sintofahamu kwa wadau wa soka Barani Afrika wakidai mpira huo ulivuka mstari na lilipaswa kuwa bao halali.

Hata hivyo Mwamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Mauritania Dahane Beida aliashiria mpira haukuvuka mstari hivyo aliruhusu mchezo kuendelea kama kawaida.

Ajali: Mafuriko yasomba basi, 51 wanusurika kifo
TAMWA-ZNZ wakumbusha ulinzi wa Watoto wakati wa sikukuu