Baada ya kuishuhudia timu ya Simba SC ikishindwa kufikia malengo yake ya kutinga hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2023/24, Rais wa Heshima na Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed ‘Mo’ Dewji, amesema mwishoni mwa msimu atakutana na Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, kwa ajili ya kufanya tathimini ya kina na kukifanyia maboresho makubwa kikosi hicho.
Simba SC wametupwa nje katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, kwa jumla ya mabao 3-0 katika michezo yote miwili nyumbani lkiruhusu bao 1-0 na kisha ugenini nchini Misri, kukubali kichapo cha mabao 2-0.
Hata hivyo, Mo Dewji amesema ameziangalia mechi zote na ameona jinsi gani wachezaji walivyopambana na anaimani na utendaji kazi mzuri wa benchi la ufundi, hivyo anatarajia kukutana na kocha kwa ajili ya kuangalia mapungufu ya timu yao na kufanya maboresho.
Amesema watafanya maboresho kulingana na mahitaji ya kocha Benchikha, kwa ajili ya kuimarisha cha timu hiyo kwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa kuwatoa hatua waliyofikia na kusonga mbele katika michuano ya kimataifa.
“Naipenda Simba SC sana, inapofanya vibaya naumia, tumefanikiwa kucheza Robo Fainali mara nyingi, tutafanya mabadiliko mwishoni mwa msimu huu kuboresha kikosi chetu kwa kuleta wachezaji wenye uzoefu kwa kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi,” amesema Mo Dewji.
Ameongeza kuwa matarajio yake makubwa ni kufanya maboresho kwa msimu ujao ili waweze kufikia malengo yao, akiamini kuwa hatua ya kufika Nusu Fainali itakuwa taratibu kama ilivyo kwa hapo awali kwani hakuna mtu ambaye anaamini Simba SC ingecheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.