Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote, Bara na Visiwani waendelee kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akizindua nembo na kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano na kusema “Muungano huu ni tunu adimu na adhimu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Hivyo basi kila mmoja awe mlinzi.“
Amesema, Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano wao kutimiza miaka 60. “Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla.“
“Kama ulivyo msemo wa Kiswahili Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi Barani Afrika na duniani kwa ujumla.“
Waziri Mkuu amesema kilele cha sherehe za muungano kitafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam, hivyo ametoa wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia maadhimisho hayo.