Benki ya Biashara Nchini (TCB), inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 83 ya Hisa, inatarajia kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake ifakapo Mwakani mwaka 2025.
Benki ya TCB inatokana na historia ya mabadiliko kuanzia Tanganyika Postal Office Savings Bank (TPOSB) iliyoanzishwa mwaka 1925 Tanganyika ilipokuwa chini ya utawala wa Ukoloni Mwingereza, na mabadiliko kadhaa mpaka baadae kufahamika kama Tanzania Postal Bank mpaka Tanzania Commercial Bank (TCB).
Akizungumza kwenye kikao kazi na wahariri na waandishi wa Vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) leo Aprili 9,2024 jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara (TCB) Ndugu. Adam Charles Mihayo amesema, TCB imepitia katika hatua mbalimbali ambapo baadaye ilikuwa Benki ya Akiba chini ya lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika ya Mashariki (EAP&TC) na ilikoma kufanya kazi baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kisha Shirika la Posta na Simu Tanzania (TP&TC) lilianzishwa ili kuhudumia soko la Tanzania.
Baadae, TPB iliundwa kutoka kwa TP&TC ambapo ilianzishwa kwa Sheria ya Benki ya Posta Tanzania Na. 11 ya mwaka 1991. June 29, 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliifuta sheria hiyo na Machi 29, 2016 benki hiyo iliunganishwa chini ya Sheria ya Makampuni ( Sura ya 212) kama TPB Bank PLC.
January 19, 2017, benki ilizindua jina la TPB Bank PLC kwa umma pamoja na nembo yake mpya na July 14, 2021 benki ilibadilisha jina na kuwa Tanzania Commercial Bank Plc.TCB inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hisa asilimia 83.44, Shirika la Posta hisa asilimia 7.61, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hisa asilimia 2.91. Huku, Simu Savings and Credit Cooperative Society Limited hisa asilimia 2.67,Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF hisa asilimia 2.35 na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) hisa asilimia 1.02.
Nae Afisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho amesema, lengo la vikao hivyo ni kuondoa ukuta au pazia ambalo wengi walihisi taasisi zo za umma zimejifungia ndani na na zinafanya mambo yake kimya kimya.
“Na hata changamoto zinapotokea na ikatolea umma umepewa hizo taarifa mapokeo yake ni tofauti,” amesema Sabato huku akifafanua kuwa,
Baada ya vikao kazi hivi ambavyo vimewapa Watanzania mwanga wa kile kinachoendelea ndani ya taasisi na mashirika ya umma, wamekuwa na uelewa mpana na hata taarifa zinapotoka wanakuwa hawana maswali mengi.
Mihayo ameongeza kuwa, TCB inahudumia Watanzania wa makundi zaidi ya milioni mbili, na ina lengo la kukua kibiashara na huduma, mwaka huu itatoa mikopo ya Sh bilioni 300 kwa wafanyabiashara na wajasiriamali 2,000 ikiwa na dhamira ya kuwa benki namba tatu kwa ukubwa nchini.
Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Hazina imewapongeza wanahabari kwa kuendelea kuwa na mchango chanya katika kufikisha elimu kwa umma kuhusu yale yanayofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali ya umma nchini.
Amesema, vikao hivyo vinatoa fursa kwa taasisi na mashirika ya umma kueleza yalipotoka, yalipo, yanapoelekea na mafanikio yake kwa ujumla.