Lydia Mollel – Morogoro.
Viongozi wa dini wametakiwa kuwa wa kwanza kukemea uvunjifu wa maadili katika jamii kwa kushirikiana na wazazi kutoa mafunzo stahiki kwa vijana kujilinda, ili kupunguza wimbi la vitendo viovu.
Kauli hiyo, imetolewa na Mwalimu Augustine Tengwa ambaye amesisitiza umuhimu wa jukumu lao katika kupinga vitendo viovu katika jamii, akiwataka kuwa mstari wa mbele katika kukemea mwenendo unaoshuhudiwa kati ya vijana.
Amesema, “unakuta Kijana wa kiume amesuka nywele ,amevaa hereni hana tofauti na mke wake haya mambo tusipokemea sasa yanazidi kukua tutakua na kizazi cha hivyo baadaye.”
Aidha, ameitaka Serikaliwa kwa kushirikiana na watu maarufu, Viongozi wa dini kupanga mikakati ya kuzunguka nchini nzima kwenye nyumba za ibada na maeneo mengine ya umma kuelimisha jamii kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na biashara haramu ya binadamu.
Naye Nassoro Boazi, ameongeza kuwa ushirikiano wa Wazazi, Serikali, Wadau, na Viongozi wa dini ni muhimu katika kulinda maadili na kuzuia mwenendo mbaya wa kizazi kijacho, ili kupata jamii bora na kuzalisha viongozi shupavu.