Serikali imeingilia kati mgogoro uliopo kati ya Viongozi wa Soko la Machinga la Old Airport na Viongozi wa Shirikisho la Umoja wa machinga – SHIUMA, Jijini Mbeya uliokuwa ukiathiri ukuaji wa Soko na kudhoofisha maendeleo ya Wafanyabiashara Sokoni hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa akizungumza na Viongozi hao amesema Wamachinga wanapaswa kutumia fursa ya uwepo wa soko hilo na kuwaletea tija, hivyo ni vyema kuepuka migogoro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wa soko hilo, Shadrack Mwamwenda amesema changamoto iliyopo inatokana na viongozi wa SHIUMA kuingilia maamuzi wanayoyatoa, hivyo kukwamisha utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayotolewa, kuchafuliwa pamoja kuwagombanisha na Wafanyabiashara.
Akitoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa SHIUMA, Jerry Mwatebela amesema Uongozi wa sasa wa Soko hilo umekuwa ukifanya vitendo vya ubadhilifu wa mali za Wamachinga, ikiwa ni pamoja na kumiliki baadhi ya maeneo na kufanya ujenzi bila utaratibu na kutoshirikisha shirikisho kuhusu uamuzi yanayowahusu Wamachinga.
Kufuatia hali hiyo, DC Malisa amepanga kukutana na machinga, ili pia aweze kuwasikiliza kwa lengo la kupata ufumbuzi sahihi wa changamoto iliyopo.