Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema limekuwa likitenga zaidi ya Shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuhudumia Wajasiriamali wadogo katika kuweka mazingira wezeshi kwa Wafanyabiashara na Wazalishaji Mbalimbali nchini, ili weweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na ushindani.
Hayo yamebainishwa hii leo Aprili 15, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi mkuu wa TBS, Athumani Ngenya wakati akiwasilisha Ripoti ya Utendaji kazi wa Shirika hilo ndani ya Miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, hadi kufikia sasa TBS imetoa mafunzo kwa makundi mbalimbali takribani 5,789 ikiwemo Wajasiriamali wadogo (MSEs) na Wazalishaji wengine ili kuwasaidia kuzalisha Bidhaa zinazokidhi matakwa ya Viwango vya Ubora na Usalama ili kukidhi Masoko ya ndani, kikanda na kimataifa ili kukuza biashara na uchumi.
“Katika kipindi cha miaka mitatu, Leseni za Ubora wa Bidhaa 2,106 tulizitoa kwa Wazalishaji mbalimbali wa bidhaa nchini, ikiwa ni saw ana asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2000,” amesema Ngenya.
Kuhusu usajili wa Bidhaa za Chakula na Vipodozi, Ngenya amesema TBS hudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kwa kutumia mfumo wa ‘PVoC’ Pamoja na kufanya ukaguzi kipindi bidhaa zinapowasili nchini.
“Ndani ya Miaka mitatu, tulikagua Jumla ya Shehena 100,851 kabla haijaingizwa nchini ikiwa ni saw ana asilimia 99 ya lengo la kukagua Shehena 102,083, ambapo jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya zilikaguliwa baada ya kuingia nchini ikiwa ni saw ana asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417” amefafanua Ngenya.
Aidha katika hatua nyingine, akizungumza na Dar24 Media Ngenya ameeleza kuwa TBS imeshinda Tuzo ya ubora wa kudhibiti ubora Afrika kwa kushika namba moja na kwa kuzishinda Nchi 54 za Afrika.