Kocha wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Miguel Gamondi amesema hana presha na mchezo ujao wa Ligi kuu dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba.
Young Africans itaikaribisha Simba SC Jumamosi (Aprili 20) katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha Gamondi ameweka wazi kuwa, hana presha na mchezo dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi Simba na ataiandaa timu yake vyema kupata ushindi na kuiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa taji.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesisitiza kuwa, tayari ameanza mipango ya mchezo dhidi ya Simba SC lakini hatokuwa na Presha yoyote juu ya wapinzani wake na anauchukulia mchezo huo kama mechi zingine katika ligi hiyo.
“Kweli ni mchezo maalumu, lakini kwangu ni kama mchezo mwingine, naheshimu timu zote hivyo hata maandalizi ni sawa (na timu nyingine), tumemaliza hatua moja sasa tumeanza kujiandaa na mchezo huu, sina presha yoyote. Nitaiandaa timu na kujaribu kupata ushindi,” amesema.
Gamondi amesema sababu kubwa ya timu yake kuwa tishio msimu huu ni ubora, kujituma na nidhamu ya kimbinu inayoonyeshwa na wachezaji wake.
“Kuwa na wachezaji bora ambao wanacheza kwa umoja na kujituma, kuwa na nidhamu ya mbinu, hawa wachezaji wanacheza kama familia na ni jambo la muhimu,” amesema.
Young Africans inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 55 baada ya kushuka dimbani mara 21, huku Simba SC ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 46 katika michezo 20.
Timu hiyo ya wananchi itaingia katika dabi ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-1 iliyoupata dhidi ya Simba SC katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.