Magwiji wa soka Tanzania wamebashiri mchezo wa Jumamosi (Aprili 20) ambapo mabingwa watetezi Tanzania Bara Young Africans watakuwa wenyeji kwa kuwaalika Simba SC.
Young Africans na Simba SC zitarudiana kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku nyota wa zamani wa soka wa Tanzania wakitabiri mchezo mgumu kwa pande zote mbili.
Kujiandaa na mchezo huo mabingwa watetezi Young Africans ambao ni wenyeji wa mchezo huo wameamua kubaki Dar es salaam huku wapinzani wao Simba SC wakitimkia visiwani Zanzibar jana Jumanne (Aprili 16).
Beki wa zamani wa Young Africans Bakari Malima amesema utakuwa mchezo mgumu kwa timu zote mbili na hakuna timu yenye uhakika wa asilimia 100 ya kuondoka na ushindi kwenye mechi hiyo.
“Tunatakiwa kusubiri na kuona nini kitatokea baada ya filimbi ya mwisho lakini kwa sasa ni ngumnu kutabiri nani atakuwa mshindi kwenye mechi hii,” amesema Malima aliyewahi pia kuitumikia Pan African kabla ya kujiunga na Young Africans.
Malima amewaomba mashabiki wa timu zote mbili kulinda amani kwenye mchezo huo kwani soka ni mchezo wa kiungwana.
“Bila kujali kama umeshinda au kufungwa, muhimu kukubali matokeo na kuweka malengo ya kupata ushindi kwenye mchezo unaofuata, hii ni ari kwa mashabiki wa timu zote mbili wanatakiwa kuwa nayo ili kufanya mchezo wa soka kuwa wa kuvutia,” amesema
Kwa upande wake beki wa zamani wa Majimaji ya Songea, Sigara na Mtibwa Sugar, Abdul Ntila amesema lolote linaweza kutokea kwenye mchezo huo kwani kila timu ina wachezaji wazuri wanaoweza kuwapa ushindi wakati wowote.
“Tusisahau timu zote mbili zina wachezaji wenye ubora na mabenchi yao ya ufundi yanaundwa na makocha wenye uzoefu mkubwa. Hii inatosha kukuonesha mchezo utakuwa mgumu kiasi gani kwa timu zote mbili.”
“Sehemu yoyote ile duniani hakuna mechi rahisi kati ya timu mbili zenye upinzani mkubwa, hii itakuwa mechi bora ya msimu na tutarajie mechi yenye ushindani mkali na timu itakayokuwa imefanya maandalizi yake vizuri itapata ushindi,” amesema Ntilla
Young Africans inaongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 55 kwenye mechi 21 walizocheza huku Simba SC ikishika nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 46 katika mechi 20. Azam FC wanashika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 22 wakifikisha pointi 50.