Lydia Mollel, Rufiji – Pwani.

Wananchi walioathiriwa na mafuriko  Wilayani Rufiji wameiona thamani na umuhimu wa uwepo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA baada ya kupokea misaada mbalimbali kutoka kwa taasisi hiyo  yenye thamani ya shillingi millioni 20 ikiwemo tani 6.4 za unga wa sembe, Kilo 666 za maharage na magodoro 186.

Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA akimkabidhi misaada hiyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, Kamishna Msaidizi mwandamizi Abraham Jullu amesema TAWA imeguswa na janga la mafuriko lililowapata majirani na wadau namba moja wa uhifadhi wananchi wa Rufiji ambao wamehusika kwa kiasi kikubwa kulinda rasilimali za Hifadhi ya Selous na hivyo imelazimika kuwashika mkono.

Jullu amesema tangu changamoto hii ya mafuriko imejitokeza TAWA ilifika kwa haraka na kuongeza nguvu kwa kutoa kikosi cha Askari 24  ili kusaidia katika zoezi la uokozi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya mbinu za kujikinga na madhara yatokanayo na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko kwa jamii ambapo mpaka sasa TAWA imetoa elimu hiyo kwa wananchi wapatao 4,225 na bado inaendelea na zoezi hilo.

Sanjari na hilo, TAWA imetoa boti moja lenye uwezo wa kubeba jumla ya watu 15 ili kusaidia katika shughuli za uokozi zinazoendelea wilayani humo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amemshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda kwa maamuzi ya haraka waliyoyafanya kupeleka misaada hiyo kwa wananchi wa Rufiji kwa wakati.

Aidha, ameishukuru TAWA kwa msaada wa boti kwa ajili ya kufanya shughuli za  uokozi na ushiriki wao wa ujumla katika zoezi la uokozi kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya dola na kukiri kuwa wananchi wa Rufiji wanaona thamani na umuhimu wa uwepo wa Taasisi hiyo Mkoani Pwani.

Licha ya kuishukuru TAWA, Mkuu wa wilaya ya Rufiji Meja  Edward Gowele amesema TAWA imekuwa na mahusiano na mashirikiano mazuri kati yake na uongozi wa wilaya yake ndio maana imekuwa rahisi kwao kuitikia wito wa kutoa msaada kufuatia janga lililoikumba wilaya hiyo.

Young Africans Vs Simba SC shilingi imesimama
Chanjo HPV kuwakinga Wasichana saratani mlango wa kizazi