Dereva wa Basi dogo la Shule ya Msingi Ghati Memorial, lililosombwa na maji na kuua wanafunzi nane jijini Arusha, Lukuman Hemed amepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka nane, likiwemo la kuua bila kukusudia.
Waendesha mashtaka wa Serikali, Yunis Makala na Amina Kiango wamesema Mshtakiwa huyo aliendesha gari aina ya Toyota hiace namba T496EFK April 12 2024 bila kuchukua tahadhari na kuzingatia usalama wa Abiria aliowabeba waliokuwa chini ya uangalizi wake.
Wamesema, mstakiwa pia aliliendesha gari hilo kwenye maji ya mvua eneo la Engosengiu, Sinoni na kushindwa kulimudu kulikopelekea kusombwa na kusababisha vifo vya Wanafunzi nane wenye umri wa miaka kati ya mitatu na kumi na tatu.
Aidha, dhamana ya dereva huyo imepingwa na mawakili hao kwa madai ya kuwa usalama wake uko hatarini kutokana na wananchi kuwa na hasira na dereva huyo aliyesababisha ajali, japokuwa hakimu alitangaza dhamana kuwa wazi.