Boniface Gideon – TANGA.

Shirika la Amend Tanzania kwakushirikiana na Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga chini ya ufadhiri wa Ubalozi wa Switzerland Nchini, wameendesha zoezi la utoaji wa Elimu ya Usalama Barabarani kwa Madereva Daladala na Bodaboda Jiji la Tanga, ikiwa ni sehemu ya kupunguza na kutokomeza ajari za Barabarani zinazotokana na uzembe wa Madereva.

Akizungumza wakati wa utoaji wa Elimu hiyo iliyofanyika katika Stendi ya Pongwe jijini hapa, Ofisa Miradi kutoka Amend Tanzania, Scholastica Mbilinyi amewaambia Waandishi wa Habari kuwa, lengo ni kuwafikia Madereva 500 na mpaka sasa Madereva 300 tayari wameshafikiwa katika awamu ya Kwanza.

Amesema, “tumeshawafikia Madereva 300 wa pikipiki maarufu kama Bodaboda,tumewapatia mafunzo ya Usalama Barabarani na waliohitimu tumewapa vyeti ,hivyo tunaendelea na zoezi hili la kutoa Elimu ya Usalama Barabarani na awamu ya pili itaanza mwezi mei mwaka huu na itakuwa endelevu.”

Scholastica aliwataka Madereva wa vyombo vyote vya moto kuzingatia sheria za Usalama Barabarani ili kupunguza ajari za Barabarani zinazotokana na uzembe wa Madereva, huku Mkuu wa Usalama Barabarani,kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga ( R.T.O ) Mrakibu wa Polisi ‘SP’ Willy Mwamasika, akiwataka Madereva wote kwenda Darasani kama sheria inavyowataka kufanya hivyo.

Aidha, aliwaonya Madereva wa Daladala kuacha tabia ya kusimamisha Daladala zao kwa muda mrefu kwenye maeneo yasiyokuwa na vituo katikati ya Jiji hili lenye mpangilio mzuri wa namba za Barabara za mitaa.

Ajali basi la Shule Arusha: Dereva apandishwa kizimbani
Mashanda: Wakandarasi msijifungie, tokeni mjifunze