Zaidi ya tani 200,000 za korosho ghafi, zimesafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara katika msimu wa mwaka 2023/2024.
Akizungumza kwenye mkutano wa Wadau wa maendeo wa ushoroba uliofanyika mjini Mtwara, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kijavara amesema mafanikio hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Septemba 2023.
Amesema, Korosho ghafi kutoka Mtwara zilikuwa zinasafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam lakini kuanzia msimu wa 2023/2024, Korosho zimekuwa zinapitia Bandari ya Mtwara baada ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika Bandari hiyo ikiwemo kuongeza vifaa vya kisasa za kupakia na kupakua mizigo na idadi ya Wafanyakazi.
Kuhusu Ujenzi wa Bandari maalumu kwa mzigo mchafu ya Kisiwa Mgao, Mhandisi Kijavara amesema Mkandarasi wa ujenzi wa Bandari hiyo ameshapatikana na kwamba ujenzi unatarajia kuanza Mwezi Mei 2024, na utatekelezwa kwa miezi 24.
Awali, Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini, Devotha Gabriel alisema ushoroba wa Mtwara ni lango kuu la biashara na uwekezaji kwa ukanda wa kusini na Tanzania kwa ujumla na ukiendelezwa ipasavyo utaleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya Wananchi