Kocha Mkuu wa mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, Young Africans, Miguel Gamondi amesema bado timu hiyo haijawa bingwa pamoja na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mtani wake wa jadi Simba SC, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi Jumamosi (Aprili 20).
Ushindi huo unaiacha Young Africans kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi saba dhidi ya Azam iliyo na mchezo mmoja zaidi na pointi 12 dhidi ya Simba SC yenye mchezo mmoja mkononi.
Gamondi amesema wamebakiwa na mechi saba kabla ya kutangazwa kuwa mabingwa na wanatakiwa kucheza mechi zao zote kutetea taji lao.
“Hauwezi kuwa na uhakika na kitu chochote kwenye maisha na zaidi kwenye soka…bado tuna mechi saba… ni kweli tuna tofauti ya pointi kubwa lakini bado tunatakiwa kucheza mechi zote. Falsafa yangu ni kwenda hatua kwa hatua na leo tumepiga hatua kubwa lakini usisahau Jumanne tuna mechi na Alhamisi tuna mechi,” amesema Gamondi
Amesema ulikuwa mchezo mgumu na kila timu ilicheza kwa kujituma na kuongeza anajivunia kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake.
Amesema walistahili kupata ushindi ambao kwa mujibu wake, ni wa mashabiki na wazee wote wa timu hiyo.
Naye Kocha Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola amesema ulikuwa mchezo mgumu ambao wachezaji wake walitengeneza nafasi za kufunga walizoshindwa kuzitumia.
“Mechi ilikuwa nzuri na ngumu, tulitengeneza nafasi za kufunga kipindi cha kwanza lakini wachezaji wetu walishindwa kuzitumia na nafikiri bado tuna tatizo la kushindwa kutumia nafasi kwenye mechi zetu,” amesema Matola
Amesema mabadiliko ya lazima yalitokana na kuumia kwa beki wao, Henock Inonga na yaliwagharimu kwani beki chipukizi, Hussein Kazi alifanya makosa yaliyowapa Young Africans Penati waliyofunga bao lao la kuongoza.