Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ na Shirikisho la Soka Visiwani Zanzibar ‘ZFF’ wamekubaliana kurejesha michuano ya Kombe la Muungano baada ya miaka 20.

Mashindano hayo yanarudi rasmi wakati Tanzania inasherehekea miaka 60 ya Muungano ulioasisiwa na Julius Nyerere akiwa Rais wa kwanza wa Tanganyika na Abeid Anmaan Karume wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF kupitia Ofisa Habari wake Clifford Ndimbo, mashindano hayo yataanza kesho Jumanne (Aprili 23) na yatashirikisha timu za Simba SC na Azam FC kutoka Tanzania Bara na mabingwa wa Zanzibar, KMKM na KVZ.

“Timu za Simba SC na Azam FC zote zimeshiriki kuthibitisha mashindano haya. TFF na ZFF zinawaomba Watanzania wote kushirikiana kufanikisha mashindano hayo kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu.” amesema Ndimbo

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Azam FC amesema timu yao inatarajia kuelekea Zanzibar kesho Jumanne (Aprili 23) kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika Uwanja wa New Amaan Complex.

Timu za Simba SC na KMKM zimeshiriki mara nyingi michuano hii miaka ya nyuma huku ikiwa ni mara ya kwanza kwa Azam na KVZ.

Kombe la Muungano lilianza mwaka 1982 na kufa mwaka 2003 huku Young Africans wakiongoza kwa kushinda ubingwa huo mara sita na Simba SC mara tano, Majimaji mara tatu, Malindi wamechukua mara mbili huku Pan African, KMKM, African Sports, Pamba na Tanzania Prisons zikichukua mara moja moja.

MALIMWENGU: Tamaduni tano za kushangaza Ulimwenguni
Gamondi: Tumepiga kwenye mshono, lakini bado